Connect with us

General News

Wanasiasa wafufua magenge ya uhalifu – Taifa Leo

Published

on


Wanasiasa wafufua magenge ya uhalifu

NA WAANDISHI WETU

MAGENGE yanayothaminiwa na wanasiasa yameanza kuchipuka katika kila pembe ya nchi, hali inayotishia usalama wa kitaifa pamoja na uchaguzi huru na wa haki.

Uchunguzi wa Taifa Leo umegundua kuwa wanasiasa wa mirengo tofauti ya kisiasa wamefufua makundi ya uhalifu huku wengine wakianzisha mapya kwa lengo la kutisha wapiga kura na kukabili wapinzani wao.

Katika Kaunti ya Murang’a, makundi kadhaa yamechipuka na yanakodishwa kuzua fujo.

Baadhi ya makundi hayo ni Nja Nene, Gwata Ndai, Lakers na Holy Basilica.

Mnamo Jumapili, magenge mawili yanayohusishwa na wawaniaji ugavana Irungu Nyakera na Joseph Wairagu yalikabiliana katika eneo la Gaturi ambapo watu 12 walijeruhiwa na magari ya wapinzani kuharibiwa.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, Naibu Kamishna wa eneo la Kati, David Ndege alisema waliofanya jaribio la kutibua mkutano ulioongozwa na mwaniaji urais mwenza wa Azimio, Martha Karua ni wanachama wa genge ambalo linajiita Wasame.

Aliyekuwa mshirikishi wa mpango wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi aliambia Taifa Leo kuwa magenge hayo hufadhiliwa na wanasiasa na yamezagaa katika maeneo mengi ya nchi.

“Makundi haya hufufuliwa na wanasiasa wakati wa uchaguzi. Baada ya kura kuisha yanarudi mashinani kuhangaisha wananchi hadi uchaguzi ujao yanapotumika tena na wanasiasa. Wengi wa wanasiasa wanatumia makundi haya ya wahalifu. Mengi huongozwa na wahalifu sugu ama maafisa wa usalama waliostaafu. Wakati wa uchaguzi unakuwa ndio msimu wao kuvuna pesa,” akasema Bw Kaguthi.

Katika maeneo ya Pwani, polisi wamekuwa wakilaumu wanasiasa kwa kufadhili magenge yanayozua fujo za kisiasa mara kwa mara.Watetezi wa haki za binadamu katika Kaunti ya Mombasa jana walidai kuwa ripoti walizokusanya tangu Januari zimeonyesha watu 14 wamefariki katika ghasia za kisiasa.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Haki Africa, Hussein Khalid alitaka polisi wachunguze wanasiasa wanaochochea ghasia hizo.

Katika juhudi za kuzuia kuimarika kwa makundi hayo, polisi wameongeza katika baadhi ya mitaa inayohangaishwa na magenge ya wahalifu msimu huu wa kisiasa kama vile Kisauni, Nyali na Likoni katika Kaunti ya Mombasa.

Katika eneo la Nyanza, makundi ya vijana ambao wanakodishwa kwa Sh500 kwa siku yamechipuka, ambapo yanatumiwa kutekeleza maagizo ya wanasiasa ikiwemo kuvuruga mikutano ya wapinzani na kutisha wananchi.

Katika Kaunti ya Homa Bay, maafisa wa usalama wanachunguza kisa ambapo wafuasi wa wawaniaji wa ugavana Gladys Wanga na Evance Kidero walipigana mnamo Jumapili. Watu saba walijeruhiwa na mali ya thamani kubwa kuharibiwa.

Katika Kaunti ya Kisii kumekuwa na visa vya ghasia baadhi ya wawaniaji viti wakishambuliwa kwa mawe. Baadhi ya wanasiasa eneo la Kisii wanalaumiwa kwa kuchochea vijana kutatiza mikutano ya wapinzani wao.

Ongezeko la visa vya uhuni wa kisiasa katika eneo hilo vimelazimisha maafisa wa usalama kufanya vikao na wagombeaji katika juhudi za kuzuia hali kuzorota zaidi.

Katika Kaunti ya Migori, Mbunge wa Suna Magharibi Peter Masara alishambuliwa mwezi uliopita na wafuasi wa mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi ujao, Joseph Ndiege.

Maafisa wa usalama katika kaunti hiyo wamefichua kuwa wanafuatilia magenge 10 ambayo yanatumiwa kuzua fujo za kisiasa.

Kati ya makundi hayo ni Sangwenya, ambalo linajumuisha wanawake na wanaume ambao wanakodishwa na wanasiasa kuwapa huduma kama vile kudumisha usalama katika mikutano yao na pia kushambuliwa wapinzani.

Duru zilieleza kuwa kundi hilo limepata ujasiri hivi kwamba linapanga shughuli zake kwenye mitandao ya kijamii ambayo pia linatumia kutisha watu.

Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Migori, Meru Mwangi alisema wanafanya kila juhudi kuhakikisha makundi hayo yanazimwa uchaguzi mkuu ukikaribia.

Ripoti ya Mwangi Muiruri, Winnie Atieno, Rushdie Oudia, Ruth Mbula, Ian Byron na George Odiwuor

 Source link

Comments

comments

Trending