Connect with us

General News

Uhuru awafaa matajiri – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Uhuru awafaa matajiri – Taifa Leo

UCHUMI: Uhuru awafaa matajiri

NA PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta wiki iliyopita, akihutubia jamii ya Mlima Kenya katika kikao cha Sagana 3, alijipiga kifua jinsi amekuza uchumi wa Kenya kutoka utajiri wa Sh5 trilioni alipoingia ofisini 2013 hadi Sh13 trilioni sasa.

Rais aliendelea kuorodhesha miradi muhimu ambayo serikali yake imetekeleza katika miaka yake 10 uongozini, ikiwemo ujenzi wa barabara, usambazaji stima, mageuzi katika sekta za ardhi na kilimo.

“(Rais) Kibaki aliniwachia uchumi wa Sh5 trilioni, nitakayempokeza serikali atapata uchumi wa Sh13 trilioni. Nimepanua uchumi kufikia Sh13 trilioni, nimejenga kilomita 12,000 za barabara, nimeunganisha Wakenya kwa stima kutoka asilimia 28 nilipochukua hatamu kwa Kibaki, hadi asilimia 78,” akasema, akiongeza kuwa chini ya uongozi wake Wakenya milioni sita wamepata hati za umiliki wa ardhi.

Aliendelea kusifu mageuzi katika sekta ya Kilimo tangu alipomfuta aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri mnamo 2020 na kumteua Peter Munya anayehudumu hadi sasa, akisema wakulima wa kahawa, majani chai na mpunga wamenufaika pakubwa.

“Wakulima wa mpunga ambao hawakuwa na uwezo wa kuuza mazao kwa kuwa mchele ulikuwa ukinunuliwa kutoka Pakistani sasa wanauzia serikali mchele. Hawa wa Mwea wamelipwa zaidi ya Sh600 milioni, ambazo mbeleni zilikuwa zikienda Pakistani,” Rais akasema.

SIASA Hata hivyo, hotuba ya Rais ambayo kwa upana ililenga kuwapiga kisiasa wapinzani wake wakiongozwa na naibu wake, William Ruto, haikuwapa wananchi taswira kamili ya hali halisi. Hii ni kutokana na kuwa alikosa kufafanua kuwa japo anajigamba kukuza uchumi wa Kenya, wale ambao wananufaika na maendeleo yake ni matajiri wachache ambao wamezidi kutajirika huku idadi ya maskini ikiongezeka.

Ripoti mbili za utafiti ambazo zimetolewa mwaka huu, moja na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) na nyingine na mashirika mawili ya kuheshimika – Oxfam na Development Finance International (DFI) – zimeeleza kuwa karibu Wakenya milioni 10 wametumbukia katika umaskini chini ya uongozi wa Rais Kenyatta huku pengo kati ya maskini na matajiri likipanuka zaidi.

KNBS iliripoti kuwa idadi ya Wakenya maskini ilipanda kutoka asilimia 38 ya taifa mnamo 2014 hadi asilimia 53 mnamo 2018. Hii ni kumaanisha kuwa wakati wa uongozi wa Rais Kenyatta, idadi ya Wakenya maskini imepanda kutoka milioni 17.7 mnamo 2014, mwaka mmoja tu baada yake kuingia uongozini, hadi milioni 27.2 mnamo 2018 kulingana na rekodi za Benki ya Dunia.

Mashirika ya Oxfam na DFI yaliripoti kuwa Wakenya wawili matajiri zaidi wanamiliki mali nyingi zaidi ya inayomilikiwa na jumla ya Wakenya maskini milioni 16, hali inayodhihirisha kuwa manufaa ya maendeleo ya serikali yanawaendea wenye pesa, huku yakizorotesha hali ya maskini.

“Umaskini nchini Kenya umevuka mipaka. Japo uchumi unakua vyema tangu 2005, umaskini bado unaathiri maisha ya mamilioni ya watu. Inaonekana kuwa matajiri wachache na wawekezaji ndio wanavuna matunda ya kukua kwa uchumi, lakini matunda haya hayawafikii maskini,” shirika la Oxfam linasema.

UCHUMI KUTEGEMEA MADENI

Kati ya utajiri wa Sh8 trilioni ambao Rais anasema ameongezea taifa, Sh7 trilioni ni madeni aliyokopa kufadhili miradi ambayo mingi imebainika kutonufaisha Wakenya moja kwa moja, na ambayo kiasi kikubwa kimeporwa na wafisadi serikalini.

Wakati wa uongozi wake, kiwango cha madeni ikilinganishwa na utajiri wa taifa kimepanda kutoka asilimia 38 hadi asilimia 68.

Afisi ya Kushauri Bunge kuhusu Masuala ya Bajeti (PBO) mwaka jana ilikadiria kuwa madeni ya serikali yatatimu Sh8.8 trilioni kufikia Juni mwaka huu, huku serikali ikikadiriwa kutumiwa Sh1.36 trilioni kuyalipa kuanzia Julai 2022.

Hii ni kumaanisha kuwa kuanzia Julai, mzigo wa madeni kwa serikali utakuwa umepanda kwa asilimia 77 zaidi, kutoka Sh765 milioni zilizotumika kuyalipa mwaka wa 2020/21.

USHURU WA JUU

Ili kuweza kuyalipa, serikali imekuwa ikitoza bidhaa muhimu na za matumizi ya kawaida ushuru wa juu, hali ambayo imewaacha wananchi wakiteseka kutokana na ugumu wa maisha, ndiposa umaskini unakolea.

Watafiti pia wameonya kuwa kuna uwezekano kuwa serikali itashindwa kutimiza majukumu muhimu kama vile kufadhili sekta za elimu, afya na kuwakinga wasiojiweza katika jamii kwa misaada ya pesa, kutokana na mzigo wa madeni unaendelea kupanda.

Wameonya kuwa serikali imekuwa ikipunguza ufadhili kwa sekta ya kilimo ambayo inategemewa na mamilioni ya Wakenya, hali ambayo imepunguza uzalishaji wa sekta hiyo na kuzidisha umaskini.

Katika sekta ya kawi, japo serikali imesambaza stima kwa mamilioni, umaskini pamoja na bei ya juu ya stima kutokana na ufisadi katika kampuni ya Kenya Power vimewaacha wengi bado wakiteseka, huku rasilimali za mabilioni zilizotumiwa kusambaza stima zikiwa hazitumiki.

Kwa jumla, japo utajiri wa taifa umepanda, maisha ya Mkenya wa kawaida hayajashuhudia mabadiliko makubwa.

Wataalamu wanasema serikali ya Jubilee imewekeza zaidi wanaponufaika matajiri na kutelekeza ambapo hali ya maisha ya maskini ingeboreshwa.