Joho akubaliwa kufuliza mamilioni kulipa mishahara
WINNIE ATIENO NA ALEX KALAMA
BUNGE la Kaunti ya Mombasa limekubalia utawala wa Gavana Hassan Joho kuchukua mkopo wa Sh484 milioni.
Pesa hizo zimenuiwa kutumiwa kulipa mishahara ya zaidi ya wafanyakazi 2,000 wa kaunti hiyo ambayo imekuwa ikichelewa kwa sababu ya changamoto za kifedha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Bajeti na Matumizi, Hamisi Mwidani, alisema kaunti haina budi ila kukopa ili kulipa wafanyikazi wake.
“Kama mishahara haitalipwa, itaathiri huduma za kaunti,” alisema.Kando na mishahara, pesa hizo zimenuiwa pia kugharamia malipo ya ada zinazokatwa kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi kila mwezi ambazo zimesemekana hazijakuwa zikiwasilishwa kwa asasi husika kwa miezi kadha sasa.
Wahudumu wa afya walifanya mgomo baridi Januari 8 kulalamikia masuala hayo lakini wakarudi kazini wakati walipolipwa Januari 10.
MALALAMISHI
Miongoni mwa malalamishi yao ilikuwa kwamba ada kama vile za Bima ya Afya ya Kitaifa (NHIF) zilikuwa haziwasilishwi kwa asasi husika ilhali hati zao za mishahara zinaonyesha pesa hizo zilikuwa zinakatwa kila mwezi.
Kwingineko, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kaunti ya Kilifi, Bw Albert Kiraga, ameitaka bodi ya kuajiri wafanyikazi katika bunge la kaunti hiyo kuelezea kuhusu madai ya kuwepo kwa tangazo la kuhitaji wafanyikazi zaidi.
Akizungumza katika kikao cha bunge la kaunti hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Bw Kiraga alidai kuwa kwa sasa bunge hilo lina wafanyikazi 128, idadi ambayo alidai ni kinyume na ile inayohitajika kwa mujibu wa kanuni za Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC).
‘Inashangaza sana kuona ya kwamba kumetolewa tangazo la kuhitaji wafanyakazi zaidi ilhali bunge hili tayari lina wafanyikazi wengi zaidi walioajiriwa ambao hata wamepita ili idadi hitajika,’ akasema Bw Kiraga.
UFAFANUZI
‘Tunataka ufafanuzi zaidi kutoka kwa bodi hii itueleze kwa undani ni kwa nini inafanyika hivi. Kwa sababu kuajiri wafanyikazi wengi kupita ile idadi hitajika kulingana na utaratibu uliowekwa ni ukiukaji wa sheria,’ akazidi kusema.
Kwa upande wao wanachama cha Kadu Asili wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa chama hicho, Bi Anne Sidi walisema kitendo hicho cha kutaka kuajiri wafanyakazi zaidi kinatiliwa shaka.’Hiyo mambo ya kuajiri watu hasa wakati huu ambapo muhula wa gavana unakaribia kuisha sawa na spika haifai,’ akasema Bi Sidi.
Next article
Kaunti yalenga kusafisha maji ya bahari