Connect with us

General News

Kaunti yalenga kusafisha maji ya bahari – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kaunti yalenga kusafisha maji ya bahari – Taifa Leo

Kaunti yalenga kusafisha maji ya bahari

NA WINNIE ATIENO

SERIKALI ya Kaunti ya Kwale, imeanzisha mashauriano na kampuni tofauti za kigeni ili kutafuta jinsi ya kusafisha maji ya baharini kwa matumizi ya nyumbani.

Gavana wa kaunti hiyo, Salim Mvurya, akiandamana na maafisa wengine wa kaunti walifanya mazungumzo na kampuni ya Acciona Agua iliyo na makao yake makuu Uhispania ili kutafuta mwongozo kuhusu jinsi mpango huo unaweza kutekelezwa.

Kampuni hiyo inanuia kusafisha maji ya bahari kwa ushirikiano na ile ya Swicorp kutoka Saudi Arabia.

Wawekezaji wa makampuni hayo waliohudhuria mkutano huo mwishoni mwa wiki iliyopita, walitaja eneo la Munje lililo katika eneobunge la Msambweni kuwa mwafaka kwa utekelezaji wa mradi aina hiyo.Walieleza uwezo wa kujenga kiwanda kwenye ekari 50 ya ardhi Kwale.

Kiwanda hicho kimekadiriwa kitagharimu takriban Sh19 billion na kuzalisha takriban lita 150 milioni za maji kwa siku.

“Tutaendelea kushirikiana kwa minajili ya kuimarisha Kaunti ya Kwale. Lengo letu ni kuhakikisha miradi hiyo inanufaisha wakazi na bei ya maji kuwa chini zaidi,” akasema Bw Mvurya.

Miradi sawa na hii ilikuwa imeanzishwa katika maeneo mengine ya Pwani kama vile Kaunti za Mombasa na Lamu, ila haijapiga hatua kubwa kufikia sasa.

Endapo mradi huo utafanikiwa, utapiga jeki miradi mingine inayoendelezwa na serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na kaunti ambayo pia inalenga kuboresha usambazaji wa maji safi kaunti hiyo pamoja na zile zinazopakana nayo.

Serikali kupitia kwa Wizara ya Maji iliwekeza mabilioni ya pesa kwa ujenzi wa mabwawa Kaunti ya Kwale katika miaka iliyopita na miradi hiyo ingali inaendelezwa.Wakati uo huo, sekta ya afya katika kaunti hiyo inatarajiwa kuimarika baada ya kaunti kutia saini mkataba na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID).

Gavana Mvurya na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo anayesimamia ukanda wa Afrika Mashariki, Bw Mark Andrew Meassick, walisema mkataba huo utakuwa muhimu kwa uboreshaji wa huduma za afya kwa umma.

‘Hii ni historia ambayo itaipiga jeki sekta ya afya, ninashukuru USAID ambayo imefanya kazi ya serikali ya kaunti ya Kwale hapo awali katika sekta za afya na vijana. Serikali yangu imeweka miundomsingi bora kwa kujenga zahanati 150, kutoka 34 ambazo zilikuwa hapo awali na kununua vifaa, dawa na kuajiri maafisa wa afya,’ alisema Gavana Mvurya.

Kwa upande wake, Bw Meassick aliipongeza serikali ya Bw Mvurya kwa kuwekeza katika afya.Katika miezi ya hivi majuzi, sekta ya afya kaunti hiyo ilipata pigo baada ya madaktari, wauguzi na maafisa wengine wa afya kufanya mgomo kwa takriban wiki mbili.

Migomo hiyo iliyotaka kushinikiza malipo ya marupurupu na kupandishwa vyeo kwa wahudumu wa afya, ilikuwa pigo kwa juhudi za kaunti kuhakikishia umma huduma bora za afya.